Kiungo wa zamani Yanga na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Ali Mayai ametazama mechi ya Simba dhidi ya Mtibwa juzi na kusema hazitishi kwani zina udhaifu mkubwa katika idara ya ushambuliaji.
Timu hizo ziliumana mwishoni mwa wiki katika pambano la Ligi Kuu lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Simba iliidungua Mtibwa mabao 2-0.
Akizungumza mtandao huu Mayai alitaja upungufu wa idara za ushambuliaji za timu hizo kuwa ni washambuliaji wa timu hizo kukosa ubunifu wanapoingia eneo la hatari.
“Ukweli ni kwamba Simba na Mtibwa zina udhaifu mkubwa eneo la tatu yaani ushambuliaji,” alisema Mayai.
Alisema, “Mtibwa na Simba zinacheza vizuri kuanzia nyuma mpaka katikati, lakini mpira ukifika pale mbele hakuna la maana linalofanyika, hauoni mashuti yakipigwa wala nafasi za maana za kufunga zinazotengenezwa.”
Alisema hata mabao mawili ya Simba yalipatikana kutokana na uzoefu na uwezo binafsi wa wachezaji Henry Joseph na Betram Mombeki, lakini siyo mipango ya kiuchezaji.
“Inawezekana mtu akahoji Simba ilishindaje kama haikucheza vizuri, lakini ukweli ni kwamba uzoefu na uwezo binafsi wa mchezaji kama Henry Joseph na hata yule Mombeki ndiyo ulisaidia na siyo mbinu za kiuchezaji,” alisema Mayayi ambaye pia ni mchambuzi wa soka.
Hata hivyo, Mayai alisema Simba na Mtibwa zina fursa ya kufanya vizuri katika ligi inayoendelea kama zitarekebisha udhaifu katika safu zao za ushambuliaji.