Licha ya muda mrefu kupita tangu mauzo ya Okwi yalipofanyika, Simba haijapokea hata senti moja kutoka Etoile zaidi ya kuambulia ahadi zisizotekelezeka.
Akizungumza na mtandao huu jijini, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope alisema klabu yake inakusudia kuishtaki Etoile kwa Shirikisho la Soka Kimataifa endapo fedha hazitalipwa hadi Septemba 31 mwaka huu.
“Tumeshawaandikia barua ya kuwakumbusha kuhusu malipo ya fedha zetu Dola 300,000, lakini kama hawatatulipa hadi kufikia Septemba 31 tutawashtaki Fifa,” alisema Hans Pope na kuongeza:
“Wametuambia wameipata barua yetu na wanalishughulikia suala hilo, hivyo sisi tunawasubiri wasipotekeleza huo ndiyo msimamo wetu.”
Ili kuhakikisha klabu yake inalipwa deni hilo, Hans Pope alisema wameiunganisha Etoile na klabu ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini ambayo alidai imeonyesha nia ya kumsajili Okwi.
“Tumewasaidia sana Etoile hadi kufikia hatua ya kuwaunganisha na Ajax na timu nyingine ya Uturuki ambayo siikumbuki ili wamuuze Okwi, tunafanya hivi ili akiuzwa sisi tupate chetu,” alisema Hans Pope.