come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA, MBEYA CITY KURUDIANA

Uongozi wa klabu ya Yanga jana umewasilisha rufaa kwa shirikisho la soka nchini (TFF) kuomba mchezo wao dhidi ya Mbeya City urudiwe katika uwanja huru kutokana na vurugu zilizotokea kabla na baada ya kuanza kwa mechi hiyo iliyoishia kwa sare 1-1.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, ofisa habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema kuwa baada ya kutokea vurugu za kushambuliwa kwa basi lao wakati likiingia uwanjani kabla ya kuanza kwa mechi hiyo,  walitoa taarifa kwa wasimamizi wa mchezo huo, kamishna wa mechi, Mhagama, msimamizi wa mchezo huo, Charles Ndagala.

“Yanga hatuwezi kugomea mechi yoyote japo zile vurugu ziliwaondoa mchezoni wachezaji wetu, tuliandika barua kuomba kwa kamishna wa mchezo na msimamizi tucheze mchezo chini ya pingamizi (under protest)," alisema Kizuguto.

Alisema kuwa Yanga haitaki Mbeya City wakatwe pointi badala yake wanataka mchezo huo urudiwe katika uwanja huru.

Aliongezea kusema kuwa mbali na vurugu hizo pia hawakuridhika na maamuzi ya mwamuzi Andrew Shamba aliyechezesha mchezo huo kutokana na kasoro zilizojitokeza.

“Mwamuzi hakuwa makini na kazi yake, alishindwa kuumudu mchezo, mfano alikataa goli halali lililofungwa na Kavumbagu (Didier) katika dakika ya 60 kwa madai golikipa wa Mbeya City aliguswa wakati akichezea mpira…, lakini mashabiki na ninyi wanahabari mmeona kilichotokea, golikipa yule alikuwa akileta mbwembwe mara baada ya kudaka mpira na wakati akifanya mbwembwe hizo mpira ulimtoka na Kavumbagu akafunga, lakini mwamuzi alikataa…, hayo ni sehemu ya mapungufu ambayo sisi kama Yanga tumeona yamechangia kupata matokeo ya sare,” aliongeza Kizuguto.

Aidha, alisema kuwa Jumatano wanacheza na Prisons katika uwanja huo lakini uongozi wa Yanga hauna imani tena na hali ya usalama katika uwanja huo na wanahofia kufanyiwa tena vurugu.

“Huu uwanja umeshaonekana hauna ulinzi…, tunashauri au tunaomba TFF waamishe mchezo huu ili uchezwe kwenye uwanja mwingine wenye usalama ili kuepuka vurugu kama hizi zilizotokea dhidi ya Mbeya City,’ alisema Kizuguto.
Alisema kuwa wachezaji wao wameathirika kisaikolojia kutokana na vurugu katika uwanja huo hivyo wana hofu hawatakuwa katika viwango vyao kwenye mchezo wa Jumatano.

Kizuguto alisema vurugu zilizotokea katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mbeya City umeisababishia hasara timu hiyo ya Sh. 2,900,000 baada ya kuvunjwa kioo cha basi la wachezaji.

Pia mashabiki hao walivunja kioo cha nyuma cha gari ndogo aina ya Noah yenye namba za usajili T 618 BQU iliyokuwa ikitumiwa na viongozi wa klabu hiyo mjini hapa.

Wakati huo huo, mechi ya Jumamosi baina ya Yanga na Mbeya City iliingiza kiasi cha Sh. Milioni 100  kutokana na kuhudhuriwa na mashabiki 20,000.

Katika mgao wa mapato hayo kila klabu ilipata kiasi cha Sh 23.6 huku fedha nyingine zikienda kwenye gharama za mchezo na makato mengine.