Wanachama wa Yanga wameikataa Azam Tv kurusha mechi zao na kuwataka viongozi wao kuipeleka mahakamani kama itakaidi na kuendelea kurusha mechi za Yanga bila idhini ya klabu hiyo.
Wanachama hao wa Yanga walitoa tamko hilo la kuikataa Azam Tv jana wakati wa Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam.
Akiomba ridhaa ya wanachama wake kwenye mkutano huo kuhusu Azam Tv kuonyesha mechi za Yanga, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuph Manji aliwataka wanachama hao kutoa uamuzi kuhusu mkataba wa Azam Tv.
Manji alisema, “Azam Tv wanataka kuonyesha mechi zetu kwa gharama ndogo ya Sh 100 milioni kwa mechi 26 tunazocheza ligi nzima, hiyo ni sawa na Sh3 milioni kwa kila mechi, kiasi hicho cha fedha ni kidogo kwa kuwa mechi moja ya Yanga inaingiza zaidi ya Sh3 milioni na ile inayohusisha Simba huwa tunapata zaidi ya Sh100 milioni.”
Baada ya kutoa mchanganuo huo Manji aliwahoji wanachama kama Azam Tv kuonyesha mechi zao kwa kiasi hicho ni halali au sio halali, ambapo wanachama hao walijibu,“Sio Halalii, mkataba wa Azam hautufa! Hatutaki fedha zao.”
Naye Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga alisema,“Kuna kampuni ambayo tumeingia nayo mkataba SGM ya nchini Kenya kwa ajili ya kuonyesha mechi yetu ya raundi ya kwanza dhidi ya Al Ahly ya Misri, kampuni hii kwa mechi moja tu dhidi ya Al Ahly inatupa Dola 55 elfu (sawa na Sh90 milioni).”
Alisema,“Tulikubaliana na Azam Tv wao wabaki na kipindi cha Yanga Soccer Show, sisi tuendelee na Haki zetu za Televisheni na Zuku, lakini yaliyotokea hapo katikati yanajulikana, wanachama wameamua tuwapeleke mahakamani Azam Tv, lakini sisi kama viongozi tutakaa na uongozi mpya wa TFF kuliangalia upya suala hili pamoja na wanasheria wetu, milango bado ipo wazi kwa Azam Tv kukaa nasi tena na kuzungumza upya suala hili.”
Ujenzi wa Uwanja wa Kaunda
Akizungumzia suala la ujenzi wa Kaunda, Mwenyekiti anayeiongoza kamati hiyo ya ujenzi, Francis Kifukwe alielezea dhamira ya uongozi wa Yanga kujenga jengo la kisasa litakalojulikana kama Jangwani City Mall, pia akaweka wazi kwa kusema,
“Kiwanja chetu kina hati miliki kwa miaka 99 tangu mwaka 1972, hati ya kiwanja hiki ilitumika kuchukua mkopo na kukabidhiwa Benki ya Nyumba mwaka 1973, katika mazingira yasiyoeleweka hati hiyo imepotea na vyombo husika vilijulishwa, nakala ya hati hiyo ya zamani tunayo, uongozi umelipa deni hilo Sh100 milioni ikiwa ni malimbikizo ya kodi ya kiwanja, Wizara imeahidi kupitia upya tathmini ya makadirio ya malimbikizo ya kodi ya kiwanja yalipwe ili hati nyingine itolewe badala ya ile kupotea.”
“Kwa sasa tumewasilisha barua kuomba ongezeko la hekta 11 tunasubiri Manispaa ya Ilala kutoa eneo la nyongeza ndipo ujenzi uanze,” alisema Kifukwe.